Maendeleo mazuri
Tarehe 16/4/2024 ilikuwa siku nzuri kwa Chuo cha Kilimo na Mifugo Igabiro. Wajumbe wapya wa bodi ambayo ni kwa mujibu wa mwongozo wa NACTVET walizindua bodi hiyo. Tumefurahi chuo kina wanachuo 300 hadi sasa. Changamoto iliyopo kwa sasa ni miundo mbinu. Kimsingi maendeleo ni mazuri.
Vijana wetu 11 wako Israel kwa mazoezi ya vitendo na wengine 6 wameajiriwa huko na tumetaarifiwa kuwa wote wako salama na wanaendelea vizuri. Mwaka huu pia 2024 tutachagua wengine wa kupeleka nchini Israel.
Pamoja nao walikuwa ni wajumbe wa “Special Purpose Vehicle” ambao walikutana mara ya kwanza kujadili na kuweka mpango kuhusu Mradi wa Uboreshaji shamba la Mifugo ambao umeanza kutekelezwa awamu ya kwanza kutokana na vyanzo vya ndani. Katika hatua hiyo Chuo kinalenga kuinua kiwango cha maziwa yanayopatikana kwa kununua ng’ombe breed nzuri inayotoa lita kuanzia 10 na kuendelea kwa siku. Tayari ng’ombe 5 wenye mimba wamenunuliwa toka Kahama flesh na kuletwa Igabiro, na wameanza kuzaa. Ng’ombe wengine 5 watanunuliwa na kuletwa Igabiro hivi karibuni. Pia ng’ombe 20 ambao wako Igabiro tangu mapema wamepandishwa kwa artificial insemination ili tupate breed nzuri inayotoa maziwa mengi kama wataalam wanavyotwambia kuwa tabia ya kutoa maziwa mengi inatoka kwa Dume. Haya yote yamefanyika kwa kutumia vyanzo vya ndani.
Hatua ya pili ya mradi itahusisha kupata ng’ombe wengi zaidi ambao wana sifa ya kutoa maziwa ya kutosha ili ndani ya miaka 5 tufikie:
1. Kuwa chanzo cha maziwa katika wilaya ya Muleba
2. Mahali pa kuuza mitamba
3. Chuo ambacho kinaweza kufundisha wanachuo kwa vitendo zaidi ili nao wakajitegemee
4. Kiwe kituo kikubwa cha Internship ya wanachuo kutoka vyuo vikuu. Wafike kupata mazoezi ya vitendo
Wajumbe walitembelea miradi mbali mbali chuoni na kikao kilifikia mwisho kwa furaha.